Hakimiliki ya picha: Soka la Bongo
SIMBA imekutana na ugumu wa kumpata kiungo mshambuliaji wa Klabu ya RS Berkane ya nchini Morocco ambayo imegoma kumuachia.
Adebayor ni kati ya wachezaji waliokuwa katika mipango ya muda mrefu ya Simba ya kumsajili tangu msimu uliopita.
Simba imepanga kufanya usajili mkubwa wa wachezaji watakaowafikisha hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya misimu mitatu kuishia Robo.
Mmoja wa mabosi wa Simba, amesema kuwa kwa mara ya pili Simba wameifuata Berkane kwa ajili ya mazungumzo mapya ya kumsajili kiungo huyo ambaye amemalizana na uongozi wa Msimbazi iliyopanga kumsajili katika msimu huu.
Bosi huyo alisema kuwa katika mazungumzo hayo, Berkane imeonekana kuendelea na msimamo wake wa kumbakisha hapo licha ya kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Aliongeza kuwa Berkane imekataa kumuachia kiungo huyo kwa mkopo kwenda Simba ambayo ilipeleka maombi hayo kumtaka kiungo huyo mwenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi.
“Berkane imeendelea na msimamo wake wa kiungo wao mshambuliaji Adebayor anayehitajika na Simba kwa mkopo katika msimu ujao.
“Hii ni mara ya pili kwetu kumuhitaji Adebayor kwa mkopo, tuliwasilisha maombi hayo ya kumtaka kwa mkopo katika usajili wa msimu uliopita, pia hivi karibuni tulipeleka tena maombi.
“Yeye mwenyewe mchezaji tumeshamalizana naye, lakini tatizo ni klabu yake inayommiliki kushikilia msimamo wa kukataa kumtoa kwa mkopo,”
alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alizungumzia hilo la usajili na kusema kuwa: “Tupo katika mazungumzo na baadhi ya wachezaji tutakaowasajili katika msimu ujao ambayo yapo katika hatua nzuri mara baada ya kukamilika tutaweka wazi.”
Msimu ujao Simba wamedhamiria kufanya kweli ambapo tayari wameshaanza safisha safisha ya kuondoa wachezaji ambao kwa misimu iliyopita hawakuwa na msaada kwao.
Kupitikia mitandao yao ya kijamii, Simba mpaka kufikia sasa wameshatangaza kuachana na Augustine Okrah, Nelson Okwa,Mohhamed Outtara, Akpan, Jonas Mkude, Erasto Nyoni pamoja naye Gadiel Michael.
Taarifa za ndani zinadai kuwa bado list hiyo itaongezeka, ambapo inatazamiwa Sawadogo, Onyango, Peter Banda na Moses Phiri huenda wakafuata.
Kwa misimu miwili mtawalia, Simba wameshindwa kufua dafu mbele ya Yanga ambapo wamegalgazwa kuanzia kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA, mbaya zaidi wakashudia Yanga wakienda hatua ya fainal ya CAF.