STAA ALIYEPIGWA CHINI AZAM FC AIBUKIA SIMBA SC


Hakimiliki ya picha: Soka la Bongo


Wakati wakiwa wamebaki wachezaji wawili tu kujiunga kambini nchini Uturuki, uongozi wa Klabu ya Simba SC umeendelea kukiboresha kikosi chao kuelekea msimu mpya wa 2023/24, kwa kufanya usajili mwingine wa mchezaji wa ndani.
 
Tayari wachezaji wote waliosajiliwa wamewasili kambini Uturuki isipokuwa Fabrice Ngoma na Clatous Chama, ambao walitarajiwa kuondoka leo Jumatano (Julai 19) kwenda kujiunga na wenzao kambini kujiandaa na msimu mpya.
 
Tayari Simba SC imesajili wachezaji wapya wanne wa kimataifa katika dirisha hili kubwa, ambao ni kiungo mkabaji Fabrice Ngoma raia wa DR Congo, beki Mcameroon Che Fondoh Malone, kiungo mshambuliaji Willy Essomba Onana (Cameroon) na winga Aubin Kramo (Ivory Coast).
 
Huku kwa upande wa wachezaji wa ndani ikiwa imekamilisha na kumtangaza beki wao pembeni wa zamani, David Kameta ‘Duchu’ pekee.
 
Hata hivyo, Simba SC ambayo itakuwa na kazi ngumu msimu ujao ikiwa inakabiliwa na michuano minne mikubwa, miwili ya ndani, Ligi Kuu na Kombe la FA na idadi kama hiyo kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi ya Soka Afrika (Africa Super League), imedaiwa kunasa saini ya mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Mtanzania Shaban Chilunda.
 
Chilunda aliachana na Azam FC baada ya mkataba wake kuisha na sasa chanzo chetu ndani ya klabu hiyo kimetueleza kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba SC kwa msimu wa 2023/24 wa mashindano mbalimbali yaliyopo mbele yao.
 
Chanzo hicho makini kutoka ndani ya timu hiyo, kimesema kuwa, usajili wa wachezaji wazawa unaendelea na Chilunda amemalizana na Simba SC na muda wowote kuanzia sasa ataungana na mastaa wenzake waliopo Uturuki.
 
Kimesema: “Tunatambua ubora wa Chilunda, tunaamini kwa wachezaji wazawa ataongeza nguvu ndani ya kikosi, tumeshakamilisha usajili wa nyota wawili wa ndani bado tuna nafasi moja, mpango wetu ni kuongeza nguvu eneo la beki wa kati na kutakuwa na ongezeko la nyota wa kigeni.”
 
Kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni ambao kwa sasa tayari wametimia 12 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Bara, chanzo hicho kimesema, “wapo baadhi wanatarajiwa kutolewa kwa mkopo na kuuzwa kwa sababu kuna ofa ziko mezani ikiwamo ya Pape [Sakho].”
 
Kimesema baada ya Simba kukosa mataji misimu miwili mfululizo na kushindwa kufikia lengo la kutinga hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu ujao wanataka kufanya vizuri na kuirudisha timu kwenye ushindani kimataifa.
 
“Uongozi kwa ujumla haujafurahishwa na kukosa mataji yote misimu miwili mfululizo, tumeamua kukutana na kukubaliana kufanya usajili mkubwa ambao utatubeba kwenye mashindano yote tunayotarajia kushiriki,” kimsema chanzo hicho.
 
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah Try Again’, amesema hivi karibuni kuwa wanaendelea kufanya usajili mzuri na bado kuna vifaa vingine vinatarajiwa kutambulishwa.
 
“Wachezaji wapya wapya wanaendelea kuwasili kambini, nawakumbusha tu hatujamaliza kusajili furaha zaidi itakui ja hivi karibuni.” amesema Try Again.
 

Jisajili na Betway, burudika na kila tukio na amsha amsha ukibashiri kwenye ligi za mpira wa miguu kama; Ligi Kuu ya Uingereza, La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na mengi zaidi.

Kwa habari zote za michezo, taarifa za kubashiri na promosheni tufuatilie Betway kwenye kurasa zetu za FacebookTwitterInstagram na Youtube. Pakua App ya Betway.


 
 

Published: 07/19/2023