Matazamio ya Afrika kwenye Olimpiki wiki hii


Hakimiliki ya picha: Getty Images
 

Michezo ya Olimpiki 2020 

Tokyo, Japan
July 23 – Agosti  8, 2021   
 
Mwanariadha wa Burkina Faso Fabrice Zango anatarajiwa kushiriki hatua ya mchujo kuruka umbali mara tatu (Triple Jump) kwenye michezo ya Olimpiki inayoendelea nchini Japan, Agosti 3.
 
Mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 28 ndiye anayeshikilia rekodi ya dunia katika mchezo huo wa kuruka umbali mara tatu, aliyoiweka mwaka huu wa 2021 kwa kuruka umbali wa mita 18.07.
 
Zango alikuwa mwanariadha wa kwanza kabisa kutoka Burkina Faso kuishindia nchi yake medali yoyote, aliposhinda shaba na kuweka rekodi ya Afrika kwenye mashindano ya Mbio za Ulimwengu, 2019.
 
Wanariadha wawili kutoka Ghana Joseph Amoah na Benjamin Azamati, pamoja na Isaac Makwala kutoka Botswana wanatarajiwa kuchuana siku hiyo pia, katika mbio za mita 200 kwa wanaume, raundi ya kwanza.
  
Amoah alivunja rekodi ya taifa ya Ghana ya mita 200 (sekunde 20:15) iliyodumu miaka 24, iliyoshikiliwa na Emmanuel Tuffour, ambaye ameshiriki Olimpiki mara tatu; na sasa anapania kutwaa medali nchini Japan.
 
“Siendi huko tu kuhesabika kama mtu aliyeshiriki Olimpiki,” Amoah alisema. “Nataka kwenda huko na kuacha alama kwa ajili ya nchi yangu, na mimi mwenyewe.”
 
Wanariadha watatu wanawake kutoka Botswana Galefele Moroko, Christine Botlogetswe, na  Amantle Montsho nao pia watakuwa uwanjani mbio za mita 400 raundi ya kwanza Agosti 3.
 
Montsho, ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia mita 400, aliwakilisha nchi yake kwenye michezo ya 2004 mjini Athenes na 2008 mjini Beijing, ambapo alifika fainali.

Agosti 7, Helalia Johannes wa Namibia atashiriki mbio za Marathon ya wanawake, akijitapa kwa medali alizoshinda katika Mbio za Ulimwengu, Michezo ya Majeshi duniani, Michezo ya Bara la Afrika na Michezo ya Jumuiya ya Madola.
 
Mwanariadha mwenzake kutoka Namibia Thomas Rainhold anatarajiwa kushiriki Marathon ya wanaume kesho yake. Alifuzu Olimpiki Tokyo baada ya kumaliza kwenye nafasi ya 28 mashindano ya marathon ya Xiamen na yale ya Tuscany Camp, Italia.
 
Mwanariadha Lelisa Desisa kutoka Ethiopia anapania kuishindia nchi yake medali ya dhahabu ya Marathon kwa mara ya kwanza tangu 2000 michezo ya mjini Sydney, wakati Gezahegne Abera aliposhinda mara ya mwisho.
 
Desisa alishinda ubingwa wa dunia kwa kukimbia muda bora zaidi msimu huu, wa 2:10:40 kwenye Mashindano ya Riadha ya Ulimwengu 2019.

 

Published: 08/04/2021